Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Ahlul-Bayt (a.s) -ABNA- Jumanne tarehe (26-08-2025), Amir Jenerali Sayyid Abdurrahim Mousavi, katika mazungumzo ya simu na Field Marshal Sayyid Asim Munir, Kamanda wa Jeshi la Pakistan, alitoa mkono wa pole kwa wananchi wa Pakistan kwa hasara na madhara yaliyojitokeza kufuatia mafuriko ya hivi karibuni na akasisitiza kuwa msaada wowote unaowezekana kutoka kwa majeshi ya Iran utatolewa kwa fahari kubwa kwa ndugu zao wa Pakistan.
Jenerali Mousavi akizungumzia uhusiano wa pande mbili baina ya Iran na Pakistan alisema: “Mahusiano mazuri sana yapo kati ya nchi hizi mbili katika nyanja mbalimbali, hususan ngazi ya juu, na hili linaweza kusemwa kuwa ni mfano wa uhusiano wa kindugu.”
Aidha, alisisitiza umuhimu wa kulinda usalama wa mipaka ya pamoja ya Iran na Pakistan na akasema: “Kwa masikitiko, harakati za makundi ya kigaidi zimeongezeka katika pande zote mbili za mpaka. Tuko tayari kushirikiana kwa ajili ya kung’oa ugaidi kutoka eneo hili na kuhakikisha usalama wa mipaka yetu ya pamoja.”
Mkuu huyo wa Majeshi ya Iran, akipongeza msimamo na uungaji mkono wa Pakistan kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika vita vya siku 12 vya kujihami, alisema: “Tunatarajia kwamba katika mwanga wa ushirikiano huu wa pande mbili, hatua za vitendo dhidi ya magaidi zichukuliwe. Ni kweli hatua fulani zimechukuliwa huko nyuma, lakini zinapaswa kuimarishwa na mapungufu yaliyosalia kufidiwa.”
“Lazima tufanye mpaka wa Pakistan na Iran kuwa mpaka wa urafiki”
Kwa upande wake, Kamanda wa Jeshi la Pakistan, katika mazungumzo hayo ya simu, akitoa shukrani kwa rambirambi za Mkuu wa Majeshi ya Iran kwa wananchi wa Pakistan, pia alitoa mkono wa pole kwa ajili ya mashahidi wa askari wa polisi wa mpakani waliouawa huko Sistan na Baluchestan.
Field Marshal Asim Munir alisema: “Tunashirikiana na ninyi kikamilifu kuhusu suala la usalama wa mipaka. Ni lazima tufanye mpaka wa Pakistan na Iran kuwa mpaka wa urafiki, undugu na maendeleo ya kiuchumi, na bila shaka kwa kushirikiana pamoja tutalifanikisha jambo hili.”
Your Comment